Ministiries

 

 

KRISMAS 2017 JIMBO KATOLIKI ZANZIBAR

ADHIMISHO LA IBADA YA MISA TAKATIFU LAFANYIKA JIMBO KATOLIKI ZANZIBAR.

FUATILIA UJUMBE WA MAHUBIRI WA BABA ASKOFU SHAO.

        Ujumbe wa Krismas 2017 ni; “HAKI INAYOJENGA AMANI KWA WOTE“


Ndugu waamini wenzangu katika safari ya ukombozi, kwa moyo wa upendo na furaha napenda niwatakieni nyote Baraka na amani za Krismas 2017.“Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza”(Isaia 9:2). Maneno haya ya kitulizo yanasikika masikioni mwetu wakati mioyo yetu ikiwa na tumaini la amani baada ya mahangaiko na madhaifu mengi. Habari ni kwamba kati yetu amezaliwa Mwokozi Masiya, maana yake mwenye mamlaka, nguvu na muweza yote. Katika hali ya mateso na mahangaiko vizazi vilitembea katika giza la mateso, manabii walifundisha, walionya na kutia watu moyo, kwamba siku za giza, mahangaiko na utumwa zitaisha na siku ya haki na furaha itafika. Ndiko wenye njaa watashibishwa, macho ya vipofu na wenye dhambi watasamehewa dhambi zao na waliotengwa  watarudishwa. Ndugu zangu, kwa wale waliopokea mwito huu kipindi cha majilio leo hawana budi kufurahi, Kwamba leo wanatembea na Emmanuel y.n Mungu pamoja nasi.

KRISMAS NI MWANZO MPYA KWA WENGI WANAOTESEKA:
Kuzaliwa kwa Kristo ni mwanzo wa mahusiano mapya na Mungu. Ni Mungu aliyeaminika kuwa mbali na shughuli za mwanadamu amekuwa mmoja kati yetu“Umwiliisho. Ujumbe huu ni mwanzo mpya, kwani Mungu yupo kati yetu-Emmanueli. Ili uwepo wa Mungu uwe nasi daima, ni lazima tushungulikie kero za wengi wanaoteseka na hasa vijana wetu. Ni kwa namna gani tutawahakikishia vijana wetu wengi waliomaliza vidato, vyio vikuu na wamefaulu vizuri, lakini kwa miaka wapo njiani wanazurura? Hili ni swali letu sote wazazi, viongozi wa dini na siasa tulio na dhamana ya kutumikia wengine. Kwa hekima na uchaji wa Kimungu, sote tunaitwa kuongoza kwa haki na ukweli na kuheshimu sura ya Mungu inayojifunua kwa kila binadamu. Tunaitwa tuwatumikie waliotupa dhamana ya kuongoza kwa kuheshimu haki zao za msingi. Hawa wana mahitaji maalumu kadiri ya hali zao.

Vijana wetu wanahitaji ajira na elimu ya kuwawezesha kuingia ktk ulimwengu wa kazi kadri ya mahitaji ya karne ya sasa. Tuliwahimiza vijana wetu wasome, wakasoma kwa bidii na kufaulu vizuri. wengi wa hawa wametoka ktk familia zenye kipato cha chini, Maelfu wanazurura mitaani, wameshindwa kuingia vyuoni kwa kukosa ada. Kuna kila ulazima wa wazazi na serekali kukaa na kuweka vipaumbele vya kodi zetu ili waliofauli waweze kujiendeleza. Ni vizuri kufanya vijana kipaumbele cha maendeleo tunayotamani. Kuna nchi sasa zinateseka kwa kukosa vijana, na zile zenye mipango mizuri vijana ni kipaumbele namba moja cha kuendeleza. Ili furaha ya Mungu Emmanuel iwe ya kweli kwetu sote ni lazima kabisa swali la vijana lishughulikiwe kwa hali zote.  La sivyo Tanzania ya viwanda itakosa wana taaluma wa ushindani. Kitendo cha raisi wa Muungano kutoa msamaha kwa wafungwa 8,153 wakati wa sherehe za uhuru kimejengea wengi wanaoteseka ktk magereza yetu matumaini. Kitendo hiki cha msamaha kitaleta mabadiliko ya maadili na nidhamu ktk magereza yetu. Wengi wataishi kwa matumaini, kwamba huenda wakati mwingine nami nikabahatika. Tunaomba juhudi za namna hii za kujengea wanaoteseka matumani, ziangalie mahangaiko ya vijana wetu wasio na ajira na malipo ya chuoni. Tuwape matumaini kwamba mwisho wa giza lao ni mwanga.

UMASKINI WA EMMANUEL KIOO CHA HAKI NA MATUMAINI:
Mungu Emmanuel alizaliwa Pangoni Betlehemu mchafu na mkiwa asiyestahili heshima,  kinyume kabisa na matarajio ya wakuu wa wakati ule. Masiya amependa kutumia umaskini wake ili awainue wanyonge. Hawa ndiyo walikuwa kipaumbele cha utume wake, alijifananisha nao kwa hali zote bila dhambi ili awaondoe ktk lindi la dhambi na umaskini wao. Asiyependa kujinyima kwa ajili ya wengine hawezi kuwa kiongozi wa kujenga matumaini ya wananchi maskini kama Tanzania. Hali ikoje kwa viongozi wetu wa dini na siasa? Wakati huu tunapotangaziwa kwamba uchumi wa nchi unapanda kwa 7% tunashuhudia umaskini mkubwa wa wengi na utajiri wa kupindukia wa viongozi. Hii ni alama kwamba uongozi wao ni mlango au fursa ya kujilimbikizia mali mbele ya wengi maskini. Mungu Emmanueli alijishusha kwa hali ya watu wake na hivyo akawaletea matumaini. Kiongozi makini na mwadilifu ni yule ambaye ni mfano wa uhalisia wa maisha ya watu wake.  ni yule  anayejinyima kwa namna zote ili awafikie wale wengi anaowaongoza.

Tunasikia viongozi wengi wanadaiwa kutaja mali zao, lakini baada ya kutaja hatusikii lolote linalofanyika! Nabii Yeremia asema; “Je umekuwa mfalme kusudi ujisifie majumba ya mierezi? Baba yako alikula na kunywa, akatenda mambo ya haki na mema, ndipo mambo yakamwendea vema. Aliwapatia maskini na wahitaji, na mambo yake yakamwendea vema, hii ndiyo maana ya kunijua mimi Mwenyezi Mungu. Lakini macho yako na moyo wako huvutwa tu na faida isiyo halali, na kumwaga damu isiyo na hatia na kudhulumu na kutenda jeuri”{Jer 22: 16-17}. Ndugu zangu viongozi kutakuwa na amani ya kweli kama kuna haki ya kweli kwa wengi. Tujifunze kujishusha na kujinyima kwa ajili ya wengi. Amani ya kweli ni ktk haki.

HAKI NA AMANI YA KWELI NI KTK MAZUNGUMZANO:
Sababu za Umwiliisho ni kumjengea tena mwanadamu uhakika kwamba hakuna mabaya au maovu yatakayoshinda neema ya Mungu ndani mwetu. Mungu amependa kuwa kati yetu ili atembee na azungumze nasi na hivyo kuleta haki na amani tunayotamani.   Huyu ni nguvu na mwanga katika giza, ndiyo maana katika kumbukumbu ya ujio wake anaagiza tuwe mwanga wa kuondoa giza la maovu na uvunjwaji wa Haki iliyo msingi wa amani. Emmanuel, Mungu pamoja nasi anatuagiza tudumishe Amani kwa kuheshimu utu wa kila Mtanzania na kuwa na mazungumzano pale mitazamo yetu ya kijamii na kisiasa inapotofautiana. Tukubali kutofautiana na tuheshimu kutofautiana kwetu. Tofauti zetu tukiziheshimu kisheria ni utajiri wa taifa letu. Tanzania imekuwa kioo cha Amani kwa sababu ya kuheshimu utu wa kila mtu na haki msingi za watu wote. Siasa safi imeipa taifa letu sifa na heshima. Tunapojipongeza kwa hili tusisahau kamwe vijana wetu 14 waliopoteza maisha huko Demokrati ya Congo kwa kulinda haki na amani ya ndugu zetu wana Congo! Raha ya milele uwape Ee Bwana…….
Ndugu zangu tujipime na tujiulize juu ya kuheshimu utu wa wale tunaotofautiana kimtazamo. Sababu za wananchi kukubali kuwa na vyama vingi ni kutoa changamoto kwa maswali msingi ya maendeleo ya watu, kuwajibisha, kufichua maovu na udhaifu wa serekali iliyo madarakani. Pamoja na madhaifu, kwa kiasi kikubwa vyama hivi vimeleta mwanga na uwazi serekalini. Matokeo na mizengwe tunayosikia juu ya chaguzi ndogo za madiwani na hata ubunge huko bara ni ishara tosha kwamba hatujafahamu maana ya demokrasia yaani kutofautiana lakini bado kubakia wamoja. Siasa ni kama mchezo wa mpira, wachezaji wakiwa uwanjani huchuana kutafuta mshindi, lakini baada mchezo wote ni marafiki.

KRISMAS TANGAZO LA UHURU KWA WANAOTESEKA:
 Umaskini wa Kristo unavunja ukuta kati ya matajiri na maskini, umaskini wake unavunja majivuno yaliyo ndani mwetu. Kristu alikubali kusikia njaa na kiu ya wale wanyonge, kwani aliyeshiba  hamjui mwenye njaa. Betlehem nyumba ya Mkate ni ashirio la mwaliko kwamba, Tunayemwadhimisha ni Mkate na matumainio ya ulimwengu na hasa wale wenye njaa. Hivyo tunachosherekea leo ni kumbukumbu ya matendo mema aliyotenda Kristu wa ahadi, lakini hayupo nasi tena kimwili, ila anataka sisi sote tunaoamini ujumbe wake tufanye yale anayoagiza. Anatualika tushughulikie maovu yanayofunika mwanga wa upendo wake. Serekali ya awamu ya tano inasisitiza sana uwajibikaji na ukusanywaji wa kodi kwa ajili ya maendeleo ya wote. Kwa mantiki ya haki anayotangaza Mungu Emmanuel huu ndiyo mwito wake kwamba sote tutende kwa haki.

Kila mmoja wetu anaitwa kushiriki katika maendeleo ya nchi, hivyo swali la ulipaji kodi ni haki na lazima. Wakwepaji kodi tunaowafahamu ni wafanya biashara wakubwa, hawa ndiyo watumiaji na waharibifu wakubwa wa miundo mbinu ya nchi. Mfano mzuri ni matrela yaliyokamatwa bandarini juzi, ili yafanye kazi ni lazima yatumie miundo mbinu yaani barabara zetu, lakini hawa ndiyo wakwepaji kodi wakubwa. Kwa wale wanaodhani kuibia serekali au umma si dhambi, tunawatangazia rasmi kwamba hii ni dhambi kubwa, kwani inaumiza kizazi cha sasa na cha baadaye. Tunapendekeza watu kama hawa wafilisiwe na kunyanganywa liseni zao za biashara. Hakika hawa wangewajibishwa, giza la umaskini na kilio cha mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu lingepungua kwa kiasi kikubwa. Enyi wafanya biashara wakubwa lipeni kodi stahiki ili kupunguza janga la umaskini nchini.  


Ndugu waamini nawatakieni tena kila Baraka na neema za kutenda yote tunayosherehekea leo Krisma 2017 – Happy Christmas to you All!


Wenu ktk. Upendo wa Kristu,  Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp.

PICHA JUU NI ASKOFU AGUSTINE SHAO C.S.P.Sp WA JIMBO KATOLIKI ZANZIBAR AKIWA NA PAROKO WA KANISA KUU FR RICHARD HAKI PAMOJA NA MH. MOUDLINE CYRUSI CASTIKO WAZIRI WA KAZI, AJIRA, VIJANA, WATOTO, WAZEE NA UWEZESHAJI WA SERIKALII YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR AKIAMBATANA NA MWENYEKITI WA UWT ZANZIBAR WAKIPIGA PICHA BAADA YA ADHIMISHO LA MISA TAKATIFU. ZANZIBAR

Home.....

 

NEWS

 

 

 

Welcome to St Josph's Catholic Church in Zanzibar. This is one of the oldest Cathedral Catholic Church about 400+years ago.

It still hold its naturality, is well maintained to its original appearances.

Welcome and Pray with us for us and for all with love in Prayer.

 

Our Parish

This Website is owned by the Catholic Church of Zanzibar Tanzania ©Nov.2015

Home |search |facebook |Google|Tweeter |